Kiswahili cha Wallah Bin Wallah: Ni Mufti Kweli?

shikungigi

Naam, umesoma vyema. Sina uhakika kama wahenga wa jadi wangekubali mada kadha katika vitabu vyake. Wallah Bin Wallah ni gwiji wa kufahamika nchini kwa uandishi wake lakini kuna kero nimekuwa nayo kwa muda mrefu. Ingawaje lugha zote hubadilika mara kwa mara, kuna kuketi chini na kukubaliana wakati wa kuzibadilisha.

Kwa nini nimeamua kuongea hivi? Kwa sababu nimekerwa sana dakika chache zilizopita. Dadangu wa miaka minane ameniita nimsaidie kumaliza kazi yake ya ziada. (Kama umefikiria kuhusu Mwalimu Wanjiku uliposoma sentensi hiyo, tafadhali weka simu ama kifaa chochote kile unachotumia kusomea chapisho hili na uoshe uso wako kisha urudi ukiwa makini.) Kama kawaida, niliacha nilichokuwa nikifanya na kuangalia kitabu chake. Swali lilikuwa katika somo la saa.

Punde tu aliponiuliza swali lenyewe, nilifikiria Wambui alikuwa ameshindwa kuelewa jambo rahisi sana. Kwa hivyo nikamwambia aache uzembe na asome swali tena. Kitabu alichokuwa akitumia ni Kiswahili Mufti, Darasa la Tatu. Mara moja, dadangu alianza kulia na kusema simuelewi kwani hajui kusoma saa kwa Kiswahili. Hapo ndipo niliamua kuwa makini na kuelewa kwa nini alitatizika.

Ukurasa wenyewe ndio huu unauona hapa. Wallah Bin Wallah aliamua kuandika kitabu kinachofunza saa kwa Kiswahili kinachotafsiri Kiingereza neno kwa neno, yaani 6:15 am ni saa sita na robo.

Hazikupita dakika mingi nilipokumbuka mara kadha tuliyojibizana na mwalimu wangu wa Kiswahili miaka mingi iliyopita nilipokuwa darasa la nane. Wallah Bin Wallah hakuwa amekita mizizi katika mashule nyakati hizo kwa hivyo sisi wanafunzi wa karne ya ishirini hatukukumbwa na mkasa huu wa kizaazaa cha Wallah. Hata hivyo, mwalimu alikuwa ashapata kitabu hiki kipya na akatujulisha kuwa saa inafaa kusomwa kama vile tulivyofunzwa kwa Kiingereza.

Sikuwa na budi ila kumuuliza kwa nini waandishi wa habari huwa hawasomi saa kwa mtindo huo mpya. Mjadala ukaendela hadi somo likaisha na hatukuelewana. Mwishowe, mtihani wa KCPE uliwadia na kulikuwa na swali kuhusu saa (kama nakumbuka vizuri). Hadi wa leo sijajua kama nilipita jibu au la.

Turudi mwaka wa 2014. Nilishindwa kumwambia dadangu  anavyofaa kujibu hayo maswali. Isitoshe, ana vitabu viwili vinavyotofautiana. Kimoja sio kingine bali ni cha Wallah Bin Wallah na hicho kingine nilitumia mimi mwenyewe, ingawaje chapisho la kwanza; Mazoezi ya Kiswahili.

Je, huu ni ungwana?

Mwishowe ilimbidi babangu amempa majibu bila hata kusuluhisha swala lilokuwa mbele yetu. Nilipomuuliza kwa nini aliamua kuchukua njia rahisi badala ya kujua tutakavyo saidia Wambui, alikiri ya kwamba alikuwa amechoka. Kwa kweli mzee hawezi elewa mtindo mpya ulibuniwa wapi na lini kwa hivyo majibu aliyompa yalikuwa yanafuata mtindo wa kitambo.

Ebu jiulize, wakati Harith Salim ama Lulu Hassan wanapokuletea habari katika runinga, wanakwambia ni saa moja ama saa saba? Kwa nini Kiswahili Mufti pekee yake huhubiri injili ya kusoma saa kama inavyosomwa kwa Kiingereza?

Labda njia yake Wallah Bin Wallah ndio sahihi, labda sio. Hata labda alikuwa anafuata mtindo wa Kiarabu ambapo saa husomwa hivyo. Na kwa vile Kiarabu kinachangia pakubwa katika lugha ya Kiswahili, ninaelewa. Lakini pia lugha za Kibantu zinachangia pia, na saa husomwa tunavyofahamu wengi wetu. Shida yangu ni kwa nini hamna njia moja iliyo mkataba?

Ni muhimu kutaja kuwa kati ya vitabu vitatu vya Kiswahili anavyovitumia dadangu, kimoja tu ndicho kinachoshikilia usomaji wa saa hivi. Pia ni muhimu kuashiria kuwa, hata kama ni kitabu cha Wallah pekee kina maandishi haya juu yake “Kimeidhinishwa na K.I.E”, ni dhahiri kuwa vitabu vyote vimeidhinishwa na shirika hili.

Haya. Maswali yangu ni matatu tu. K.I.E (Siku hizi inaitwa K.I.C.D (Kenya Institute of Curriculum Development)) inawezaje idhinisha vitabu vinavyofunza mada tofauti na kutatanisha watoto wasio na hatia? Mtu mmoja anawezaje ruhusiwa kutunga mitindo inayochukuliwa na walimu ovyo ovyo bila kutiliwa maanani? Kwa nini wanaohusika katika silabasi za shule ya msingi wananyamaza tu na kuongea tu wakati swala lisilo na mbele wala nyuma kama kufunza watoto kwa lugha ya mama linapochipuka?

Nitaondoka sasa. Nina matumaini nitapata jawabu hivi karibuni. La sivyo Wambui atakua akiwa na jinamizi la kusoma saa. Kusoma saa kwa Kiingereza ama lugha yoyote ile ni ngumu kupindukia kwa mtoto wa rika yake tayari.

(Kama kuna makosa katika chapisho hili, tafadhali mniwie radhi. Imekuwa muda mrefu sana tangu niandike kwa Kiswahili kwa urefu. Mara ya mwisho ilikuwa mwaka wa 2007 nikiwa kidato cha nne. Kiswahili nilikipita lakini niliamini kwa dhati ya kuwa nilipoteza wakati mwingi sana nikisoma juu ya viambishi, lakabu na misimiati mingine nisiyofahamu sasa. Ningeandika kwa Kiingereza lakini hiyo ingekuwa kinyume na mada ninayojaribu kuwapa.)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *